Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Rais Ebrahim Raisi amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Sayyid Badr al-Busaidi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman na kueleza kwamba, hapana shaka yoyote kwamba, ushirikiano wa Muscat na Tehran unaweza kuimarisha zaidi mashirikiano ya nchi mbili hizi na kuwa na taathira katika utatuzi wa matatizo ya kieneo na kimataifa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema kuwa, misimamo ya Oman ni mizuri na madhubuti na ina tofauti kubwa na utendaji wa baadhi ya mataifa ya eneo hili la Asia Magharibi.
Kadhalika Rais Ebrahhim Raisi ameeleza kwamba, hatua ya utawala wa Oman ya kuzingatia na kuyapa umuhimu masuala ya Palestina na Yemen pamoja na masuala mengine ya eneo hili ni jambo la kuthaminiwa.
Ayatullah Raisi amesema pia kuwa, uhusiano wa Iran na Oman ni wa kuridhisha lakini katika uga wa masuala ya kiuchumi na kibiashara kuna fursa ambazo zinaweza kutumiwa na hivyo kustawisha zaidi ushirikiano huo.
Kwa upande wake, Sayyid Badr al-Busaidi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Oman amesifu na kupongeza himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mataifa jirani na kusema kuwa, kuna uhusiano mzuri baina ya Tehran na Muscat ambao katika kipindi chote cha historia umejengeka katika misingi ya kuheshimiana pande mbili, kuamianiana na ushirikiano chanya kwa manufaa ya usalama wa eneo na ulimwengu kwa ujumla.
342/